Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet
kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana
huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye
familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara,
mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.
Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa
na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo
ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha
uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi
alivyokuwa anampenda Anna.
Siku zinazidi kusonga mbele huku
wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu
kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome
pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani
wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.
Msichana huyo anafanya kila
kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye
shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza
kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja,
wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo
kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.
Zoezi hilo linafanyika kwa
mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi
wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili
wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali,
wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.
Wazazi wa Anna wanashangazwa mno
na hali duni na umaskini uliokithiri wanayoikuta nyumbani kwa akina
Jafet. Wanarejea jijini Mwanza na siku zinazidi kusonga mbele, hatimaye
vijana hao wanahitimu kidato cha sita lakini mama yake Anna hampendi
tena Jafet na anafanya kila kinachowezekana kuwatenganisha wawili hao.
Anna anatafutiwa chuo nchini
Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo
linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake
unabaki na majeraha makubwa yasiyopona.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Walifanya kila
kilichowezekana ili mradi mwisho wa siku kijana wao aweze kupona na kuwa
kwenye hali yake ya kawaida. Hawakutaka kumuona akiumwa tena, kwao,
Jafet alikuwa kila kitu. Hawakuwa na hela lakini kitendo cha kuwa
mgonjwa, hawakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima wafanye chochote
kinachowezekana ili kuyaokoa maisha yake.
Tayari walikuwa ndani ya gari kuelekea
katika Hospitali ya Bugando, ndani ya daladala, kila mmoja alikuwa
kimya, walionekana kuwa na mawazo, mioyo yao ilibeba majonzi makubwa,
walisali mioyoni mwao ili Mungu aonekane katika afya ya kijana wao.
Safari iliendelea kama kawaida,
walipofika Mwanza Mjini, moja kwa moja wakaunganisha kuelekea katika
hospitali hiyo. Walipofika, wakafuata taratibu zote na hatimaye Jafet
kuchukuliwa na kupelekwa katika chumba cha vipimo, kama walivyoambiwa
katika hospitali waliyotoka, hata hapo waliambiwa vilevile kwamba kijana
wao alikuwa na matatizo makubwa ya ugonjwa wa figo.
“Mtaweza kumtibu?” aliuliza mama Jafet.
“Hakuna tatizo, cha msingi malipo yawepo,” alijibu daktari.
Mara baada ya kulipia gharama
walizotakiwa kulipia, matibabu yakaanza rasmi. Hakukuwa na mtu
aliyeondoka kurudi nyumbani, walitaka kufuatilia hatua kwa hatua mpaka
pale ambapo madaktari wangemaliza matibabu yao.
Mama Jafet hakuweza kuvumilia, alimpenda
sana kijana wake, kitendo cha kuwa kwenye hali mbaya namna hiyo
ilimfanya muda wote kutokwa na machozi ya uchungu, alijisikia maumivu
makubwa moyoni mwake, wakati mwingine alisikia sauti moyoni ikimwambia
kwamba mtoto wake hatoweza kupona, hiyo ilikuwa safari yake ya mwisho,
angekufa.
“Hawezi kufa, Jafet hawezi kufa,” alijikuta akisema mama Jafet huku akilia.
“Kuna nini tena?” aliuliza mume wake.
“Ni mawazo, nasikia sauti ikinitisha kwamba Jafet atakufa,” alijibu mama Jafet.
“Hawezi kufa, Mungu atamponya,” alisema baba Jafet.
Hicho ndicho kilichoendelea, baada ya
saa tisa, madaktari wakawa wamekwishamaliza kumfanyia upasuaji hivyo
kutoa muda wa saa mbili kwa ajili ya mapumziko. Kila walichoambiwa
walikifanya, baada ya kukatika saa mbili, wakaruhusiwa kwenda kumuona
kijana wao, kila mmoja uso wake ukajawa na tabasamu pana.
Baada ya wiki mbili, Jafet akawa mzima
wa afya. Alitakiwa kusafiri kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kujiunga na Chuo cha Muhimbili kwa ajili ya kuanza masomo ya kitabibu.
Kwa kuwa hakuwa na fedha, akaanza
kufuatilia mkopo katika Bodi ya Mikopo kwa wanachuo na baada ya mwezi
mmoja, akafanikiwa kupata mkopo hivyo kuanza safari ya kuelekea jijini
Dar es Salaam, sehemu ambayo hakuwahi kufika zaidi ya kusikia kutoka kwa
watu tu.
*****
Usiku, William hakulala, kichwa chake
kilikuwa na mawazo mengi juu ya msichana Anna, alimpenda mno na alikuwa
tayari kwa kila kitu. Kitendo cha msichana huyo kumkatalia kiliuumiza
moyo wake, muda mwingi akawa mtu wa kujilaumu kwa kitendo chake cha
kumfuata msichana huyo na kumtongoza.
Kwa upande wa Anna, bado moyo wake
ulikuwa kwa Jafet, alimkumbuka mpenzi wake huyo, alimpenda zaidi ya
mwanaume yeyote lakini kwa jinsi William alivyokuwa akizidisha ukaribu
naye, akajikuta akianza kutekwa kimapenzi taratibu.
“Sitaki, sitaki kumsaliti Jafet,”
alisema Anna huku akijitahidi kujiongelesha ili mawazo juu ya William
ambayo yalianza kumuingia yaweze kumtoka.
Hiyo haikusaidia, maneno yake
hayakusaidia kitu chochote kile, hakutaka kumuingiza mwanaume yeyote
moyoni mwake lakini kitendo cha kuwa karibu na William, akajikuta
akianza kumpenda mvulana huyo.
Siku iliyofuata, mtu wa kwanza kabisa
kumfuata alikuwa William, mvulana huyo alifika mahali hapo na kumchukua
kisha kuelekea sehemu maalumu ya kukaa kwa wanachuo na kuanza kuzungumza
naye kama ilivyokuwa siku nyingine. Siku hiyo William hakutaka kugusia
kitu chochote kuhusu mapenzi, alijitahidi kujikaza ili mradi tu asimlize
msichana huyo.
“Anna, nashindwa kuvumilia,” alisema William, alikuwa akimwangalia msichana huyo usoni.
“Kwa nini?”
“Kwa jinsi ninavyokupenda…” alijibu William.
Hakuweza kuvumilia, moyo wake ulimsumbua
na mwisho wa siku kujikuta akimwambia Anna jinsi alivyokuwa akimpenda.
Siku hiyo alitumia uwezo wake wote kuzungumza na msichana huyo,
alimshika mkono na kuuminyaminya kama njia mojawapo ya kuweka msisitizo
juu ya kile alichokuwa akikizungumza.
Anna akaanza kumuelewa, hisia za
kimapenzi zikaanza kumkamata kiasi kwamba kuna kipindi alishindwa
kuongea zaidi ya kutoa miguno ya mahaba tu. William hakuacha, aliendelea
kuzungumza huku akiubinyabinya mkono ule, Anna akashindwa kuvumilia,
maneno aliyoongea William yakamuingia na hapohapo akajikuta akijisogeza
karibu na William, kilichofuata, wakaanza kubusiana kimahaba, hakukuwa
na mtu aliyeogopa macho ya watu waliokuwa wakipita.
Je, nini kitafuatia? Usikose
0 comments:
Post a Comment