Kinnah Phiri amesaini Mkataba wa miaka miwili kufundisha klabu ya Mbeya City ambayo imeamua kumtema Meja Mstaafu, Abdul Mingange.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuona kikosi hicho hakina mwenendo mzuri tangu kuondoka kwa Juma Mwambusi ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi chini ya Hans van der Pluijm Yanga SC.
Mara ya mwisho Phiri ambaye ameiongoza timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) mara kadhaa alikuwa Afrika Kusini akiifundisha klabu ya Free State Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo na ndiye aliyefanikisha usajili wa Mrisho Ngassa katika klabu hiyo ya Bethlehem.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amewaambia waandishi kuwa wana imani ujio wa kocha huyo mwenye uzoefu kwani utasaidia kukijenga upya kikosi chao ambacho msimu huu kimekuwa na matokeo yasiyoridhisha.
Kimbe alisema kwamba baada ya kukamilisha mazungumzo na kocha huyo mpya leo jioni anatarajiwa kuanza kazi yake ya kujiandaa kuikabili Tanzania Prisons watakaocheza dhidi yao Jumapili.
"Ni kweli tumepata kocha mpya, hatukuwa na amani pale timu ilipokuwa inafanya vibaya, tuliona tuna kila sababu ya kuboresha benchi la ufundi huku tukijipanga kuongeza wachezaji wengine mara baada ya msimu huu utakapomalizika," amesema Kimbe.
Jukumu kubwa alilopewa Phiri ni kuhakikisha Mbeya City ambayo ina pointi 17 ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi haishuki daraja.

0 comments:
Post a Comment